
UFUGAJI WA NYUKI KWA MTAJI MDOGO - MFUGAJI MBUNIFU ZANZIBAR
Umewahi kujiuliza ni kwa nini ufugaji wa nyuki unakua duniani hadi kufikia hatua ya makampuni makubwa kuwekeza katika biashara hii? Ufuatao ni ushuhuda kutoka Mwl.Moh'd; mfugaji wa nyuki kutoka Donge visiwani Zanzibar kama ambavyo alimuhadithia mwandishi wetu:-
"Naitwa Moh'd Rafii Yussuf
Donge vijibweni Mkoa wa kaskazini Wilaya ya kaskazini B
HISTORIA
Nilianza harakati hizi mnamo machi 2013
Kabla nilikuwa sielewi kabisa kama Nyuki anafugwa.
Kwa ufupi Mimi binafsi nilikuwa mtumiaji sana wa Asali kwa ajili ya tiba ya Mamawatoto wangu lakini kwa bahati mbaya sana mara nyengine nilikuwa huuziwa Asali feki hivo badala ya kutibu ilikuwa ni kuongeza matatizo.
Siku moja nilimuuliza mteja wangu ambae mara nyingi nilikuwa nikinunua Asali kutoka kwake "nnavojua mimi Asali ina msimu mbona wewe kila siku unayo? Unaipata wapi? “
Akanijibu kuwa ananunua, nikataka kujua kwa nani wapi.
Aliponieleza kuwa Nyuki wanafugwa nikaingia chakachani kutaka kujua ili nami niweze kjivunia Asali isiyo shaka mwenyewe.
Hatimae nkapata taarifa kuwa idara ya misitu Zanzibar wameanzisha mafunzo ya ufugaji Nyuki chini ya udhamini wa shirika la ZALWEDA kutoka Denmark, ingawa nilikuwa nimechelewa lakini nilianzia katika mafunzo ya vitendo moja kwa moja ambapo nilikutia wengi walioanza mafunzo wameshaacha njiani eti kwa sababu tu walitegemea wawe wanalipwa na kumbe ilikuwa ni kinyume chake, "mafunzo pila kulipa wala kulipia" hatimae nilibaki Mimi na Mwalimu tu.
Mwalimu wangu kwa jina la umaarufu "BARUAN" kutoka Muyuni Mkoa wa kusini Unguja alifahamu lengo langu akabaki nami hadi sasa.
KUHUSU MTAJI
Hili lilikuwa tatizo kubwa lakini kwa umahiri mkubwa Mwalimu wangu BARUAN alinishauri kutumia masanduku ya Tungule/nyanya ambayo ni rahisi kupatikana na mara nyengine hupatikana bila garama yeyote.Niliyavunjavunja na kuyajenga upya kwa kufuata vipimo vilivopendekezwa kwa mzinga ya Nyuki.
Baadae tena mwaka 2015 nilibahatika kupata mafunzo mwengine ya Nyuki wasiouma chini ya udhamini wa shirika la ICIPE kutoka Kenya kupitia idara ya misitu Zanzibar.
Hivi karibuni tena mwaka 2023 nimebahatika tena kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya Nyuki kama vile:- Asali, Nta, Chavua, Sumu ya Nyuki, Maziwa ya Nyuki, Gundi ya Nyuki na mkate wa Nyuki.
Mafunzo haya nayo yalidhaminiwa na Wizara ya uwezeshaji Zanzibar yakiongozwa na mtaalamu wa Nyuki maarufu "kiemi" kutoka Singida, ambapo kwa sasa mimi nimeamua kuzalisha CHAVUA, ASALI NA NTA.
Mambo ya kuzingatia.
1) Kuchagua eneo lililo salama kwa Nyuki wenyewe na binadamu pia.
2) Mizinga ya Nyuki ifuate vipimo vilivopendekezwa.
3) Kuwa na vifaa na zana zote kwa ajili ya ufugaji Nyuki.
CHANGAMOTO
Hapa kunaChangamoto kubwa 2 ambazo ni:-
a) Uhaba wa mtaji, ambapo imenifanya kuwa na wakati mgumu wa kumiliki vifaa vya kuongeza uzalishaji, na
b) mabadiliko ya Hali ya hewa/Tabianchi ambapo kwa ukanda wa kwetu imesababisha upungufu mkubwa wa uzalishaji wa Asali.
MIPANGO
Mipango yangu hapo siku za usoni ni kuboresha shuhuli za ufugaji kwa kujenga Banda na kuingiza Mizinga yote humo ili kurahisisha uvunaji wa Chavua kuepuka usumbufu wa kuroa na Mvua kwani Chavua huharibika kwa Maji.
WITO WANGU
a) Wafugaji wote tuungane na ili kuimarisha uzalishaji na kuwa na soko la pamoja.
b) SERIKALI nayo ituangalie Wajasiriamali wadogo wadogo kwani wengine tunaomba hata mikopo serikalini lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa makusudi hadi tumekata tamaa na kujilazimisha shuhuli zetu za ufugaji eyeji.
Pia nawashauri wadau wote wapende kutumia bidhaa za Nyuki kwani ni malighafi asilia na salama sana kwa mtumiaji badala ya kupenda saana bidhaa za Viwandani"
Je una maoni gani juu ya ushuhuda wa Mwl.Moh'd? Tuandikie katika comment